Amuua Mama Yake kwa Mapanga Kisa Mali za Urithi
MKAZI
wa kijiji cha Ilebelebe wilayani hapo, Ngassa Mathias (24),
anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kuhusika
na mauaji ya mama yake mzazi, Nyawamba Dohoi (61), kwa kumcharanga
mapanga kichwani hadi kufa.
Tukio
hilo limetokea Julai 11, mwaka huu majira ya saa 10 usiku, wakati mama
huyo akiwa amelala nyumbani kwake na wajukuu zake wawili.
Imedaiwa
kuwa watu wasiojulikana waliingia ndani na kumshambulia mama huyo
sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwamo kumkata kichwa kwa mapanga na
kufariki dunia.
Akitoa
taarifa kwa vyombo vya habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani
hapo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Simoni Haule, alisema chanzo cha
tukio hilo ni kuwania mali za marehemu alizoachiwa na mumewe na mtoto
huyo akidaiwa kutaka kuzimiliki.
“Tunamshikilia
mtoto wa marehemu Ngassa Mathias kwa uchunguzi wa awali, inadaiwa ndiye
mhusika mkuu wa mauaji ya mama yake mzazi kutokana na kutaka kurithi
mali ambazo mama yake aliachiwa na mumewe na upelelezi ukikamilika na
kubaini kufanya mauaji atafikishwa mahakamani,” alisema Haule.
“Natoa
wito kwa vijana kujishughulisha katika shughuli mbalimbali za
kimaendeleo ikiwamo kilimo, na kuacha tabia ya kutaka mali za mirathi na
kufikia hatua ya kutoa uhai wa wazazi wao,” aliongeza.
Aidha,
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kiloleli yalipofanyika mauaji hayo, Solo
Bundala, alisema walibaini kufariki kwa mwanamke huyo majira ya saa tatu
asubuhi na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Alisema kuwa katika kitongoji hicho kumekuwa kukitokea mauaji ya aina hiyo mara kwa mara.
No comments: