Header Ads

Rais Magufuli ateua makatibu wakuu na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),

Rais John Magufuli leo Jumapili Julai Mosi, 2018 ameteua makatibu wakuu watatu, naibu makatibu wakuu wanne.

Pia, amemteua Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), makamishna wa tume hiyo pamoja na balozi mmoja.

Akitangaza uteuzi huo leo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amesema Dk Moses Kusiluka ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ikulu. Kabla ya uteuzi huo Kusiluka alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Huyu (Kusiluka) anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Alphayo Kidata ambaye aliteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Canada,” amesema.

Amesema Rashid Tamatama ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk Yohana Budeba ambaye amestaafu. Kabla ya uteuzi huo, Dk Tamatama alikuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (Tafiri).

Kijazi amesema kwamba Meja Jeneral Jacob Kingu ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Naibu makatibu wakuu walioteuliwa ni Joseph Sokoine (Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira), Ramadhan Kailima (Wizara ya Mambo ya Ndani) , Sizya Tumbo (Wizara ya Kilimo), Mathias  Bulugulu (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi). Kabla ya uteuzi huo Kailima alikuwa mkurugenzi wa Tume ya Taufa ya Uchaguzi (NEC).

Katika uteuzi huo, Balozi Kijazi amesema Hassan Simba Yahaya ameteuliwa kuwa balozi na atapangiwa kituo cha kazi baadaye.

Rais Magufuli pia amemteua Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku Mbarouk Salim Mbarouk, Jaji mstaafu Thomas Mihayo na Omary Ramadhan Mapuri wakiteuliwa kuwa makamishna wa tume hiyo.

Balozi Kijazi amesema Mbarouk pia atakuwa makamu mwenyekiti wa NEC na kwamba tarehe ya wateule hao kuapishwa itatangazwa baadaye

No comments:

Powered by Blogger.