Serikali Yajipanga Na Bima Ya Afya Kwa Wote
Serikali
imeutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kuongeza kasi katika
kubuni mikakati na maboresho ikiwemo taratibu za kujiunga ambazo
zitawawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma zake.
Agizo
hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati akizundua Baraza la Pili
la Wafanyakazi wa NHIF mjini Morogoro ambapo amesema kuwa mwelekeo wa
Serikali kwa sasa ni kuhakikisha watu wote wanakuwa na bima ya afya.
“Serikali
ya Awamu ya Tano imeweka nguvu kubwa katika utoaji wa huduma bora za
matibabu kwa wananchi hivyo ninawaagiza muongeze kasi katika ubunifu na
maboresho mbalimbali ambayo yatakwenda sambamba na matarajio ya Serikali
ambayo ni kuwezesha wananchi wengi zaidi kuwa katika mfumo wa kupata
huduma za matibabu kwa mfumo wa bima ya afya,” amesema Dkt. Ndugulile.
Amewataka
watumishi wa Mfuko hususan Mameneja wa Mikoa kutokaa maofisini mwao na
badala yake watoke nje kwa ajili ya kuhamasisha wananchi, kuangalia
huduma wanazopata katika vituo vya kutolea huduma pamoja na
kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika maeneo mbalimbali.
Akizungumzia
utendaji kazi wa Baraza, amewataka wajumbe wa baraza hilo kutambua
wajibu wao ndani ya baraza kwa kuwa ni chombo muhimu katika kubuni na
kuweka mipango thabiti ya kuendesha taasisi ambayo ina dhamana kubwa ya
kuangalia ama kushughulikia huduma za matibabu kwa wanachama.
Amesema
kuwa kwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kuwasilisha muswada wa
sheria ambao utawezesha wananchi wote kuwa katika utaratibu wa kupata
huduma za matibabu kwa mfumo wa bima ya afya.
Akitoa
salaam za NHIF, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Bernard Konga
amemhakikishia Naibu Waziri kuwa, Mfuko unaendelea kutekeleza na kuunda
mipango ya kuongeza wigo wa wananchi kunufaika na huduma zake.
Amesema
kuwa Mwezi Julai, mwaka huu, Mfuko unatarajia kuzindua ‘Ushirika Afya’
ili kuwezesha wakulima katika vyama vyao vya ushirika kunufaika na bima
ya afya huku uundaji wa vifurushi mbalimbali ukiendelea. Mathalan,
Mpango wa kulipa michango ya bima kidogo kidogo kwa kudunduliza kwa
lengo la kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma za Mfuko.
“Tumejipanga
na hivi karibuni tutazindua huduma mbalimbali na hii yote ni mikakati
ya kuelekea bima ya afya kwa wote kwa lengo la kuwahakikishia wananchi
upatikanaji wa huduma za matibabu wakati wowote,” alisema Bw. Konga.
No comments: