Tanzania Yaieleza UNESCO Umuhimu Wa Utekelezaji Wa Mradi Wa Kufua Umeme Katika Bonde La Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge)
Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania yaeleza umuhimu wa kuendelea na mradi wa kufua
umeme katika Bonde la Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ndani ya Pori la
Akiba Selous kwenye Mkutano wa 42 wa Kamati ya Urithi wa Dunia
unaoendelea Manama, Bahrain, kuanzia tarehe 24 Juni hadi 4 Julai 2018.
Pamoja
na mambo mengine, Mkutano huu unajadili hali ya uhifadhi wa maeneo ya
Urithi wa Dunia na kutoa mapendekezo kwa nchi wanachama juu ya namna
kuboresha uhifadhi wa maeneo hayo.
Kupitia
Mkutano huu, Tanzania imeendelea kusisitiza msimamo wake kwenye Kamati
ya Urithi wa Dunia juu ya umuhimu wa utekelezaji wa mradi huo.
Ujumbe
wa Tanzania kwenye Mkutano huo umesisitiza hayo, kufuatia msimamo
uliowasilishwa na Maj. Jen. Gaudence Milanzi, Katibu Mkuu Wizara ya
Maliasili na Utalii kwenye Mkutano wa 41 wa Kamati ya Urithi wa Dunia
uliofanyika Krakow, Poland, Julai 2017.
Umuhimu
wa ujenzi wa mradi huo, uliwasilishwa pia kwenye kikao maalum kati ya
wajumbe wa Kituo cha Urithi wa Dunia, Bodi ya Ushauri kwa UNESCO –
International Union for Conservation of Nature (IUCN) na Wataalam wa
Uhifadhi kutoka Tanzania kilichofanyika tarehe 25 Juni, 2018 Manama,
Bahrain.
Katika kikao hiki, UNESCO imekubali kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha mradi huu hauleti madhara ya kimazingira.
Aidha,
wakati wa majadiliano ya ajenda ya hali ya ya uhifadhi ya Selous,
Tanzania ilieleza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza shughuli za
kiuchumi kutokana na kiwango kikubwa cha nishati ya umeme cha Megawati
2100 kitakachozalishwa.
Ujumbe
wa Tanzania ulifafanua kuwa tayari tathmini ya athari za kimazingira
kwenye mradi wa Stiegler’s Gorge imekamilika na kuwasilishwa UNESCO kwa
ajili ya upembuzi na kutumia fursa hiyo kulisisitiza Shirika la UNESCO
juu ya umuhimu wa maendeleo endelevu kwenye maeneo ya Urithi wa Dunia.
Kwa
nyakati tofauti, Tanzania ilipongezwa na Bodi ya Ushauri ya IUCN,
pamoja na Nchi Wanachama wa Kamati ya Urithi wa Dunia kutoka kundi la
Afrika ambazo ni; Angola, Zimbabwe na Uganda juu ya hatua kubwa
iliyopigwa katika kupiga vita ujangili na kuongezeka kwa idadi ya tembo
na faru katika Pori la Akiba la Selous.
Sambamba
na hilo, Serikali za Ujerumani na China zilipewa shukrani kwa kusaidia
Tanzania katika kuimarisha ulinzi na uhifadhi katika Pori hilo.
Vilevile,
nchi za Afrika ziliunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika
utekelezaji wa mradi huo na kupendekeza ushirikiano baina ya wataaalam
wa UNESCO na Serikali ya Tanzania.
Mwisho,
nchi hizo zilitoa mkazo juu ya utekelezaji wa ajenda ya maendeleo
endelevu yenye kuzingatia uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia.
Ujumbe
wa Tanzania kwenye Mkutano huo uliongozwa na Maj. Jen. Gaudence S.
Milanzi, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii na kuhudhuriwa na Bw.
Joseph Kizitto, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira; Bw.
Ali Khalil, Katibu Mkuu Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira – Zanzibar;
Dkt. Amina Amir, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utalii na Mambo ya
Kale – Zanzibar; Mhe. Samwel W. Shelukindo, Balozi na Mwakilishi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Shirika la UNESCO; na Wataalam wa
uhifadhi na Urithi wa Dunia kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
No comments: