IGP Sirro akemea uhalifu wa majini
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro ametangaza kiama kwa
maharamia na wahalifu wanaofanya uhalifu ndani ya Ziwa Victoria, maziwa
mengine na bahari ndani ya mipaka ya Tanzania akisema siku zao
zinahesabika.
Akizungumza
wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya mwezi mmoja kwa askari polisi 30
wa kikosi cha maji jijini, IGP Sirro alitaja matukio yatakayokomeshwa
ndani kipindi kifupi kijacho kuwa ni pamoja na yale ya kuvamiwa na
kuporwa kwa wavuvi ndani ya ziwa hilo linalochangiwa na nchi tatu za
Kenya, Uganda na Tanzania.
“Serikali
imejipanga kukomesha uhalifu ndani ya maji yote ndani ya mipaka ya
Tanzania; siku za maharamia ndani ya Ziwa Victoria na maeneo mengine
nchini zinahesabika,” amesema IGP Sirro
Amesema
askari waliofuzu mafunzo hayo pamoja na wengine ambao tayari wamenolewa
kukabiliana na maharamia ndani ya maji watatumika kufanya doria ziwani
kudhibiti uhalifu wa aina zote ikiwemo wizi na biashara haramu.
Katika mikakati hiyo, Serikali kwa mujibu wa IGP itanunua boti na zana za kisasa kwa ajili ya doria ziwani.
Mkuu
wa Chuo cha Wanamaji kilichopo jijini Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi
Mboje Kanga alisema pamoja na mafunzo ya nadharia darasani, askari hao
pia wamepata mafunzo kwa vitendo ndani ya ziwa na kufuzo kwa viwango vya
juu katika mapambano dhidi ya vitendo vya ujangili, uharamia, ugaidi na
aina zote za uhalifu ndani ya maji.
“Asakari
wanaohitimu mafunzo katika chuo hiki kilichoanzishwa mwaka 2011 wana
uwezo, ujuzi na ujasiri wa kupambana na uhalifu na vitendo vyovyote
haramu ndani ya mito, maziwa na bahari,” amesema Kanga
No comments: