Header Ads

Watanzania Kuanza Kumiliki Ardhi Juu Ya Ghorofa

Serikali imeandaa mpango mji mpya katika Jiji la Dar es Salaam utakaowezesha wananchi kupata hati miliki ya ardhi juu ya nyumba (ghorofani) na kuwa na haki sawa kama mmiliki wa kiwanja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Julai 27, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema lengo la mpango huo ni kuongeza upatikanaji wa maeneo kutokana na ongezeko la watu katika jiji hilo linalokadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni sita.

Waziri Lukuvi amesema pia katika mpango huo wananchi wenyewe ndiyo watakaopanga matumizi ya ardhi yao.

“Aidha, licha ya kupangwa kwa matumizi mapya ya ardhi hakuna mwananchi atakayevunjiwa nyumba yake badala yake mtu yeyote atakayetaka kuendeleza maeneo ya wananchi atatakiwa kukubaliana nao na kuwalipa fidia ili wahame.

“Hatua ya mwisho ya uidhinishaji wa mpango mkuu wowote kwa mujibu wa sheria ya mipango miji ya mwaka 2007 inataka wadau wakutane waipitie,” amesema.

Amesema baada ya kuidhinishwa kwa mpango huo wataipeleka kwa wananchi kwenye kata mbalimbali na kwenye vikao vya madiwani kisha Waziri wa Ardhi ataitangaza.

“Tumefanya hivi kwa sababu Dar es Salaam sasa inaendelezwa bila utaratibu, tumeandaa ‘master plan’ hii iwe dira ya upimaji na uendelezaji was jiji la Dar es Salaam,” amesema Waziri Lukuvi.

No comments:

Powered by Blogger.