Waziri Kigwangalla Atoa Onyo Kali Kwa Wanaochimba Madini Kwenye Msitu Wa Hifadhi Jijini Mbeya....... Aagiza Uongozi Wa Mkoa Kuwatafutia Maeneo Mbadala
Na Anthony Malegesi
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa onyo kali kwa
wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uchimbaji wa mchanga wa madini ya
dhahabu (makinikia) ndani Hifadhi ya Msitu wa Palamela katika wilaya ya
Chunya mkoani Mbeya.
Amesema
sheria za uhifadhi na mazingira hazihusu mtu yeyote kuchimba madini
katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria bila ya kuwa na kibali maalum
kutoka mamlaka husika.
Ametoa
onyo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha
Mwaoga, wilaya ya Chunya mkoani Mbeya baada ya kukagua na kuona
uharibifu mkubwa uliofanywa na wachimbaji hao kwenye hifadhi hiyo.
“Yeyote
anayehitaji kuchimba madini kwenye maeneo ya hifadhi ni sharti afuate
taratibu za kisheria ikiwepo kupewa kibali halali cha kufanya kazi hiyo,
la sivyo tutakaowakamata tutawachukulia hatua kali za kisheria” alisema
Waziri Kigwangalla.
Ili
kudhibiti vitendo hivyo visiendelee, Waziri huyo ameagiza Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuweka kituo cha kudumu cha ulinzi
katika eneo hilo ili kuwazuia wananchi watakaojitokeza kufanya shughuli
hizo za uharibifu wa hifadhi hiyo.
Amesema,
amebaini kuwa maeneo mengi makubwa ya uchimbaji wa madini katika wilaya
hiyo yamemilikishwa matajiri wachache hali inayosababisha wananchi wa
kawaida kukosa maeneo ya uchimbaji na hivyo kulazamika kuingia kwenye
maeneo ya hifadhi.
Kufuatia
changamoto hiyo, Dk. Kigwangalla ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mbeya na
Wilaya ya Chunya kuona uwezekano wa kuwapa maeneo mbadala wachimbaji
wadogowado katika maeneo ya wazi ili nao waweze kufaidika na rasilimali
hiyo na hatimaye kuepuka uharibifu wa mazingira kwa kuvamia maeneo
yaliyohifadhiwa.
Mkuu
wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala alisema kufuatia malalamiko ya wananchi
hao juu ya uwepo wa matajiri wachache waliomilikishwa maeneo hayo ya
uchimbaji, ndani ya wiki hii atamtuma Kamishna wa Madini wa Kanda na
wataalam wengine kuchunguza ukweli wake pamoja na kubaini mahitaji
halisi ya wananchi hao ili aweze kumshauri Waziri husika namna kumaliza
mgogoro huo.
Kwa
upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala Huduma za Misitu Tanzania
(TFS), Zawadi Mbwambo alisema sheria zinarubusu watu kuchimba madini
kwenye maeneo ya hifadhi kwa kufuata taratibu maalum.
Alizitaja
taratibu hizo kuwa ni pamoja na kutambua eneo husika, mmiliki wake,
kuomba leseni Wizara ya Nishati, kufanya tathmini ya athari za
kimazingira na kama itathibitika kutokuwepo kwa athari hizo, muhusika
atapewa leseni kutoka kwa Afisa Misitu wa Wilaya husika.
No comments: