Magazeti Yanayoandika Habari za Uchochezi wa Kidini, Kikabila Kushitakiwa
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema
wanaochukizwa na magazeti yanayoandika kuhusu ukabila na udini waende
mahakamani na wizara itakuwa shahidi namba moja.
Akijibu
hoja zilizojitokeza bungeni wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali ya
mwaka 2018/19 ya Sh32.45 trilioni leo Juni 26, 2018 amesema jana
kulijitokeza suala la ukabila ambalo haliwezi kubaki katika taarifa
rasmi za Bunge bila kujibiwa.
Dk Mwakyembe amesema suala hilo lilizungumzwa na mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia.
“Mbunge
ninayemuheshimu sana na mdogo wangu Mbatia, pamoja na maudhi yote
tunayoweza kuyapata, sisi viongozi tusikubali kwa njia yoyote kuwa
katika basi la ukabila na udini na tukifanya hivyo tutasahau mafanikio
makubwa tuliyoyapata hasa kujenga umoja,” amesema Dk Mwakyembe.
Amesema
mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aligusia magazeti ya
Tanzanite na Jamvi la Habari, kwamba yana ubaguzi wa Wachanga.
“Haya
magazeti yanaweza kushitakiwa na sheria ya habari kifungu cha 41 na
unaweza kuyapeleka mahakamani,” amesema waziri Mwakyembe.
Amesema,
“Kama umetukanwa wewe nenda mahakamani na sisi tukakuwa shahidi. Hivi
leo Mchaga ni nani, nani anaweza kushika jiwe na asimguse mkewe au
mjomba wake.”
Waziri
Mwakyembe amesema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipigania
uhuru wa nchi na wenye kuwaweka Watanzania katika umoja bila ukabila na
udini.
Amesisitiza wananchi kudumisha amani na umoja na kuepuka ukabila na udini.
Spika
wa Bunge, Job Ndugai akizungumza baada ya majibu ya Dk Mwakyembe
amesema, “Hili jambo la ukabila si la kuliendekeza kusema hapa, tunaweza
kusema tunadhani tunajenga kumbe tunafanya makosa makubwa.”
Ndugai
amesema, “Unaweza kujikuta unalalamika jambo fulani kumbe jamii hiyo
iko serikalini na kama kuna shida katika jambo hilo, tunong’one
pembeni.”
Spika
Ndugai amesema, “Makundi ya kisiasa na kijamii, tuendelee kuwa
Watanzania wamoja na dalili za ukabila ni mbaya. Hatuwezi kufika popote
kama tunaendekeza ukabila.”
No comments: