Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu Atoa Maagizo Mazito Hospitali ya Ocean Road
Serikali
kupitia Wizara ya Afya imeitaka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road
kuhakikisha mashine za utoaji wa huduma za mionzi ziwe zinafanya kazi
haraka iwezekanavyo ili kuweza kurudisha huduma hiyo kwa wagonjwa ambao
wengi wao ni wanawake wenye tatizo la saratani ya mlango wa kizazi.
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu wakati alipofanya ziara yake ya kikazi katika
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kukagua utoaji wa huduma za
matibabu katika hospitali hiyo na kupata fursa ya kuzungumza na wagonjwa
mbalimbali waliokuwa wakipata huduma za tiba ya mionzi hospitalini
hapo, huku baadhi yao wakilalamika kwamba wamekuwa wakitumia muda mrefu
kusubiri kupata huduma hususani za mionzi ya nje.
Vile
vile, Waziri Ummy alitembelea kitengo cha utoaji wa huduma za mionzi ya
ndani na kujionea changamoto ya kutokufanya kazi kwa mashine hizo za
utoaji wa mionzi ya ndani kutokana na kukosekana kwa vifaa vya 'transfer
tubes' na 'gyn applicators'.
"Natoa
maelekezo kwa uongozi wa Hospitali mhakikishe mnaweka utaratibu mzuri
ambao utapunguza muda kwa wagonjwa kusubiri huduma za mionzi ikiwemo
kuwepo na ratiba ambayo kila mgonjwa atajua anafika saa ngapi kupata
tiba hiyo pia fanyeni utaratibu wa kupata kifaa kilichoharibika mapema
iwezekanavyo", amesema Waziri Ummy.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt.
Julius Mwaiselage amemhakikishia Waziri Ummy kuwa atajitahidi ili vifaa
vilivyoharibika vinapatikana ndani ya siku mbili kutoka Hospitali
Bugando na pia wameagiza vifaa hivyo kutoka kiwandani nje ya nchi kwa
gharama ya Euro 43,200.
No comments: