Aliyesimamishwa na Mwigulu Nchemba kwa waraka wa KKKT Amerudi Kazini
WIKI
tatu baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba
kuutangazia umma kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vyama vya
Kijamii, Marlin Komba amesimamishwa kazi, imefahamika kuwa mtumishi huyo
alisharejea kazini.
Juni
8, Dk Nchemba aliitisha mkutano na waandishi wa habari wizarani jijini
Dar es Salaam na kutangaza kumsimamisha kazi Komba kutokana na barua
yake aliyoiandika akilitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), pamoja na mambo mengine, kufuta Waraka wa Pasaka wa maaskofu.
Katika
mkutano huo, Dk Nchemba ambaye ameachwa katika mabadiliko ya Baraza la
Mawaziri yaliyotangazwa Jumapili iliyopita, alisema barua hiyo ni batili
na haina baraka za Serikali na kwamba, ufuatiliaji ulionyesha ina
mkanganyiko wa anuani na angefuatilia kujua ni nani aliyeiandika.
Komba
jana alikuwapo miongoni mwa viongozi wa wizara ambao walimpokea Waziri
wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliyeapishwa juzi na Rais John Magufuli
kushika wadhifa huo.
Baada ya mapokezi, Komba na viongozi wengine wa wizara walikuwa na kikao na waziri huyo.
Alipotafutwa kuzungumzia kurejea kwake kazini, Komba hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, habari zinasema Komba alirejeshwa kazini baada ya utaratibu wa utumishi wa umma kufuatwa.
Awali,
baada ya barua hiyo ya Msajili kusambaa kwenye mitandao ya kijamii Juni
6, si waziri, wizara au msemaji wa Serikali aliyekubali kuizungumzia,
lakini katibu mkuu wa KKKT alithibitisha kuipokea.
Waraka
wa KKKT uliotolewa Machi 24 na uliosainiwa na maaskofu 27 ulizungumzia
hali ya kiuchumi, ukipongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kukusanya
kodi, umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika mikakati ya
maendeleo, utawala bora, demokrasia ya vyama vingi, usalama wa raia na
masuala mengine mtambuka.
Barua,
ambayo ilisainiwa na Komba kwa niaba ya msajili, ilisema chombo
kilichotoa waraka huo hakitambuliwi kisheria na kwamba ulizungumzia
masuala yaliyo nje ya malengo ya kanisa hilo na kutoa siku 10 kwa mkuu
wa KKKT kuufuta waraka huo.
Hata
hivyo, Dk Nchemba akiizungumzia alisema, “Tunawaomba viongozi wa dini
waendelee na kazi zao. Nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa
kwenye mitandao ya kijamii na wasifanyie kazi taarifa hizo.”
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza
wakati wa kikao cha viongozi wakuu wa wizara hiyo,Waziri Kangi
Lugola(watatu kulia), Katibu Mkuu, Meja Jenerali Jacob Kingu (wapili
kulia), Naibu Katibu Mkuu, Ramadhani Kailima(wakwanza kulia),aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo,Balozi Hassan Simba Yahaya(wapili
kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vyama vya Kijamii, Marlin
Komba(wakwanza kushoto).Kikao hicho kimefanyika jana,jijini Dar es
Salaam.
No comments: