Header Ads

Viongozi Wastaafu Wampa Ushauri Mzito Rais Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 03 Julai, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Marais Wastaafu, Makamu wa Rais Mstaafu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Maspika Wastaafu na Majaji Wakuu Wastaafu, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mhe. Rais kukutana na viongozi hao wakuu wastaafu na kupokea ushauri na maoni yao juu ya uendeshaji wa Serikali na mustakabali wa Taifa.

Katika mkutano huo viongozi hao wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwaita kwa lengo la kusikiliza ushauri na maoni yao, na wamempongeza kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi kifupi cha miaka miwili na nusu tangu ilipoingia madarakani.

Viongozi hao wamemshauri Mhe. Rais Magufuli kuimarisha na kujenga taasisi zinazosimamia uendelevu wa kazi nzuri zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano zikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli, mapambano dhidi ya rushwa, kuimarisha nidhamu kazini, kutilia mkazo watu kuchapa kazi, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali na utoaji wa huduma za jamii.

Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani kwa kuhakikisha haki inatendeka, kutathmini matatizo ya wananchi na kubuni mbinu za kuyatatua, kusimamia kwa ukaribu shughuli za kilimo na ufugaji ambazo zinaajiri Watanzania wengi na ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda na kuboresha kiwango cha elimu.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi hao kwa maoni na ushauri waliompa na amewahakikishia kuwa ataufanyia kazi.

Mhe. Rais Magufuli amewaeleza viongozi hao juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali hivi sasa ikiwemo kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambao umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 800 hadi kufikia Shilingi Trilioni 1.3 kwa mwezi, ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma utakaogharimu Shilingi Trilioni 7.26, kujenga mradi wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers’ Gorge) utakaozalisha Megawati 2,100 za umeme, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo na kuongeza mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea vizuri na kwamba itaendelea kutatua changamoto ambazo bado zipo kwa juhudi kubwa ili Tanzania iwe nchi nzuri kwa Watanzania wote.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaamu

No comments:

Powered by Blogger.