Ndege kubwa ATCL kufika mwezi huu
Shirika
la Ndege Tanzania (ATCL) limebainisha kuwa ndege yake mpya yenye uwezo
wa kubeba abiria 262, itawasili mwezi huu. Ndege hiyo itafanya safari
nchini kwa mwezi mmoja kabla ya kuanza safari zake rasmi kwenda Mumbai,
India.
Limesema
ikiwa nchini itafanya safari katika viwanja vya Kilimanjaro na Mwanza
kwa gharama nafuu, kwa lengo la kuwezesha Watanzania kutumia ndege yao
kwa bei ya punguzo.
Mkuu
wa Idara ya Biashara, Lily Fungamtama amebainisha hayo katika Maonesho
ya 42 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam na kueleza kuwa ndege hiyo
ina uwezo wa kwenda safari ya moja kwa moja kwa saa 18 na ya kwanza kwa
ajili ya safari za nje ya nchi kwa kuanzia na Mumbai.
Fungamtama
amesema, kabla ya mwisho wa mwaka huu, wanatarajia kupokea ndege
nyingine mbili hivyo kuongezeka kwa safari za masafa ya mbali.
Amesema,
kwa sasa shirika hilo linafanya safari ndani ya nchi katika mikoa ya
Kilimanjaro, Mwanza, Mbeya, Tabora, Kigoma, Bukoba na visiwa vya
Zanzibar huku wakifanya safari za Songea lakini kwa sasa wamesitisha kwa
ajili ya kiwanja kinafanyiwa marekebisho.
Fungamtama
amesema kwa nje ya nchi wanafanya safari za Comoro huku wakiwa na
mipango ya kuanza safari Bujumbura Burundi na Entebbe Uganda huku wakiwa
tayari kukabiliana na ushindani wa kibiashara katika sekta hiyo.
'Hatuogopi
ushindani kwani tuko imara katika kuongeza ubora wa huduma zetu,
uhakika wa safari, kupunguza kuchelewa, muda, kusitisha safari, pamoja
na usalama wa abiria na mali zao, uaminifu, maadili pamoja na kusimamia
miongozo ipasavyo,`alisema.
Alisema
shirika hilo lina wataalamu waliobobea katika kila sekta kuanzia
uongozi hadi huduma ndani ya ndege, kwani wamepikwa na chuo chao na
wengine kutoka nje ya nchi huku wakialika watu kusoma katika chuo chao
chenye wataalamu waliopitishwa na Mamlaka ya Anga..
“Watanzania
wameitikia huduma zetu hasa kwa kuwa na bei shindani, kwa kweli
wananchi wanatupa support kubwa pamoja na Rais amekuwa akitusaidia
katika kila nyanja hivyo ni vema wananchi kutumia ndege yetu ili kutunza
chetu kidumu,`alisema.
No comments: