Header Ads

Ubelgiji Yatinga Robo Fainali Kombe La Dunia..... Ilipigwa 2-0 na Japan, Ikaamka Na Kushinda 3-2

Ulihitajika moyo wa chuma kuamini Ubelgiji wangetoboa. Ilikuwa ni zaidi ya mechi ya hatua ya 16. Ilikuwa ni kufa na kupona. Ulikuwa ni ubabe. Baada ya kushuhudia wakipigwa 2-0 ndani ya dakika nne, ubelgiji waliishangaza dunia.
 
Katika mchezo mkali pengine kuliko yote yaliyoshuhudiwa kwenye fainali za mwaka huu, Ubelgiji walijikuta wakipigwa bao la kwanza katika dakika ya 48 Genki Haguchi kupiga shuti kali lililomzidi ujanja kipa wa Ubelgiji, Thibaut Coutouis kabla Takashi Inui hajaiweka Japan mguu mmoja ndani ya robo fainali, katika dakika ya 52.
 
Japan wakiamini wamemaliza biashara iliyowapeleka katika uwanja wa Rostov Don, Kocha wa Ubelgiji, Roberto Martinez alifanya maamuzi ya kijasiri ambayo mwisho wa siku yaliiokoa Ubelgiji. Mhispania huyo baada ya kuona kikosi chake kimezidiwa, aliamua kuwatoa Ferreira Carrasco na Dries Martens kwa mpigo.
 
Akawaingiza Nacer Chadli na Maroune Fellaini. Wote hawa ni warefu.

Kuanzia hapo Ubelgiji ni kama walizaliwa upya kabisa. Wakapiga mpira mwingi na kuwapoteza Samurai Blue kabisa. Katika dakika ya 69, Jan Vertonghen alipiga krosi iliyotinga nyavuni moja kwa moja.
 
Dakika tano baadaye, Fellaini akasawazisha kwa kichwa safi akiunganisha krosi ya Eden Hazard, huku la tatu na ushindi likiwekwa kambani na Nacer Chadli, kufuatia shambulizi la kushtukiza, kunako dakika ya 90. Mwisho wa siku ndio kama mlivyosikia, Ubelgiji wakashinda 3-2.
 
Licha ya kuwapa tiketi ya kuwafuata Brazil kibabe, Ubelgiji waliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufufuka na kushinda mechi ndani ya dakika 90, baada ya kutanguliwa kwa mabao mawili au zaidi, tangu Ureno wafanye hivyo miaka 52 iliyopita. Mwaka 1966, Ureno walitoka nyuma na kuinyuka DPR Korea 5-3, baada ya Korea kutangulia kupata mabao matatu ya haraka.
 
Aidha ushindi huo, unamaanisha kuwa, Ubelgiji wamefuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia mara mbili mfululizo kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, mabao mawili waliyofungwa na Japan yalimaanisha kuwa, Ubelgiji hawajawahi kumaliza mechi bila kufungwa katika mechi 12 za Kombe la Dunia, walizocheza kwenye hatua ya mtoano.

No comments:

Powered by Blogger.