Waziri Kigwangalla Awasimamisha Kazi Maofisa Na Askari Wote 27 Wa Tawa Katika Pori La Akiba Uwanda
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewasimamisha kazi
Maofisa na Askari Wanyamapori wote 27 wa Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania TAWA katika Pori la Akiba Uwanda akiwemo Kaimu
Meneja, Lackson Mwamezi kwa kushindwa kusimamia vizuri pori hilo na
kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
Hatua
hiyo imekuja ikiwa ni siku tatu tangu amsimamishe kazi meneja wa Pori
hilo, Mark Chuwa kwa tuhuma kama hizo pamoja na tuhuma nyingine ikiwemo
kushindwa kuondoa ngo'mbe zaidi ya 12,000 ambao wamedaiwa kuwepo ndani
ya pori hilo.
Pori
la Akiba Uwanda lipo katika bonde la ziwa Rukwa katika wilaya ya
Sumbawanga mkoani Rukwa na linasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Dk.
Kigwangalla amefanya uamuzi huo jana alipotembelea pori hilo sambamba
na kufanya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kilyamatundu
ambapo alipokea taarifa ya malalamiko kuhusu askari hao kupokea rushwa
kutoka kwa watu wenye uwezo na kuwaruhusu kuchunga hifadhini huku
wakiwanyanyasa masikini kwa kukamata mifugo yao.
Alifafanua
tuhuma hizo kuwa ni pamoja na kudaiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba
na kupokea rushwa kutoka kwa wavuvi wanaovua samaki Ziwa Rukwa kwa
kuwatozwa kila mmoja Sh. 100,000/- kwa mwezi na kuruhusu mifugo
kuchungwa hifadhini kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo kila mfugaji
hutozwa kati ya Shilingi milioni sita hadi saba.
Dk.
Kigwangalla pia ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
Takukuru kuchunguza mali na tuhuma za rushwa walizopewa askari wote wa
pori hilo wakiwemo watano waliotuhumiwa kwenye mkutano wa hadhara kwa
kuomba rushwa ya shilingi milioni 6 kwa ndugu Shija Imeli ili wamruhusu
kulisha mifugo yake hifadhini kwa muda wa miezi mitano.
Shija
alisema mnamo tarehe 05 Januari mwaka huu akiwa nyumbani kwake na Ndugu
Shemen Kuzenza, askari watano wa pori hilo walifika nyumbani kwake na
kumtishia kuwa endapo atalisha mifugo hifadhini wangemkamata huku
wakijua hana sehemu nyingine ya malisho hivyo wakamtaka kutoa rushwa ya
shilingi milioni 6 ili aruhusiwe kulisha mifugo yake hifadhini kwa muda
wa miezi mitano.
Alisema
walifanikiwa kuwapa askari hao jumla ya shilingi mil. 5.8 kwa nyakati
tofauti na kwamba walivyoshindwa kumalizia laki 2 zilizobakia askari hao
walikamata mifugo yao nje ya eneo la hifadhi.
Kufuatia
malalamiko na tuhuma hizo, Dk. Kigwangalla aliitisha gwaride la
utambuzi lililohusisha askari wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania (JWTZ),
askari wa usalama barabarani na maofisa na askari wanyamapori wa TAWA
waliokuwepo katika mkutano huo wa hadhara.
Shija
na mwenzake Kusenza waliweza kuwatambua askari watano wa TAWA
waliowatuhumu kuwaomba rushwa na hapo hapo Waziri Kigwangalla akawaamuru
kukabidhi silaha zao na kumuagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya
Kipolisi ya Laela, Aloyce Nyatola kuwakamata mara moja na TAKUKURU
ianze uchunguzi wa tuhuma hizo ili sheria ichukue mkondo wake na iwe
fundisho kwa wengine.
Hata
hivyo, baada ya mkutano wa hadhara, Dk. Kigwangalla aliamua kukagua
baadhi ya maeneo ndani ya pori hilo na kubaini uharibifu mkubwa
uliofanywa na mifugo huku dalili zikiwa ni kinyesi cha ng'ombe
kilichokuwa kimezagaa kila mahali.
Hapo
hapo alimuagiza Mkurugenzi Mkuu TAWA, Dk. James Wakaibara ambaye
aliwakilishwa na Mkurugenzi wa Biashara na Huduma za Utalii wa mamlaka
hiyo, Imani Nkuwi kuwasimamisha kazi wafanyakazi wote wa pori hilo na
kuleta wengine wapya wasimamie pori hilo ili kupisha uchunguzi.
"Hawa
wote wasimamishwe kazi na uchunguzi ufanyike kitu gani kilikua
kinaendelea hapa, kwanza ifanyike parade kuhusu suala la kumuomba rushwa
yule mfugaji, wabainike moja kwa moja wafunguliwe mashtaka, na hawa
wote nataka wachungunguzwe na mali walizonazo kama ambavyo imeelezwa
kuwa hawa wametumia hili pori kama kitega uchumi chao binafsi, huu ni
uhujumu uchumi" aliagiza Dk. Kigwangalla.
Wakati
huo huo, Dk. Kigwangalla ametoa siku 30 kwa wananchi wote wenye mifugo
ndani ya pori hilo kuitoa kwa hiari yao wenyewe kabla ya operesheni
maalum itakayowaondoa kwa nguvu. Alisema kama walijua pori hilo ni
shamba la bibi sasa wasahau na wajipange namna ya kutafuta malisho au
kupunguza idadi ya mifugo yao na kuanzisha miradi mingine ya maendeleo.
No comments: