Waziri Mkuu Majaliwa Ampokea Waziri Mkuu Wa Jamhuri Ya Korea
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amempokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee
Nak-yon ambaye amewasili nchini jana saa 12:30 jioni (Jumamosi, Julai
21, 2018) kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Kwenye
uwanja wa ndege, Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Korea alipokelewa pia
na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwele, Waziri wa Nishati, Dk.
Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng.
Stella Manyanya na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu Lee Nak-yon anatembelea Tanzania ikiwa ni hatua ya kuimarisha
uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Hii ni mara ya kwanza
kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kufanya ziara ya kiserikali
tangu nchi hizo zianzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.
Pia
ameambatana na ujumbe wa maafisa wa Serikali, wabunge na
wafanyabiashara wakubwa ambao watashiriki Kongamano la Kibiashara baina
ya Korea na Tanzania (Korea-Tanzania Business Forum) lililopangwa
kufanyika kesho (Jumatatu, Julai 23, 2018) kwenye hoteli ya Serena,
jijini Dar es Salaam.
Leo,
Jumapili, Julai 22, 2018, Waziri Mkuu Lee Nak Yon atakuwa na mazungumzo
rasmi ya kiserikali na mwenyeji wake pamoja na viongozi kadhaa wa
Serikali na pia kwa pamoja watashuhudia uwekaji saini mkataba wa kuondoa
hitaji la viza kwa watu wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za
utumishi (diplomatic and service passports).
Pia
ataenda Ikulu kumsalimia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. John Pombe Magufuli, atatembelea Makumbusho ya Taifa, Hospitali ya
Mnazi Mmoja na kituo cha utunzaji taarifa cha NIDA kilichopo Kibaha.
Anatarajiwa kuondoka nchini Jumatatu jioni, Julai 23, 2018.
No comments: